WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, ameagiza viwanda vyote nchini kuhakikisha vinatumia alama za utambuzi za bidhaa (simbomilia) za GS1 Tanzania.

Majaliwa alitoa agizo hilo jana wakati akifungua Mkutano wa Sita wa Wamiliki wa Viwanda na Watumiaji wa simbomilia (barcodes). Hadi sasa GS1 Tanzania ina wanachama 2,000. “Natoa wito kwa wenye viwanda kutumia GS1 Tanzania kutangaza na kuuza bidhaa zenye ubora katika maduka ya kimataifa na kwa kufanya hivyo, pia bidhaa zao zitachangia katika ulipaji wa kodi kwa usahihi,” alisema.

Alisema matumizi ya alama hiyo iwe ndiyo chanzo cha kulipeleka taifa kwenye kampeni ya kuhamasisha jamii kununua bidhaa zilizotengenezwa nchini. Waziri Mkuu alisema kama kila bidhaa itakuwa na utambuzi wa taifa kiambishi “620”, kutawezesha kuwa na takwimu sahihi za wazalishaji ambao wanatambulika.

Pia Waziri Mkuu alisema utambuzi wa bidhaa zinazozalishwa nchini ukifanyika kwa kutumia GS1 kila duka litalipa kodi kwa kila bidhaa inayouzwa na kusisitiza kwamba ‘barcodes’ ni muhimu kwa sababu zinawawezesha wajasiriamali kuuza bidhaa zao katika maduka rasmi ya nje na ndani ya Tanzania. Alisema miaka ya nyuma kabla ya kuanzishwa kwa GS1 Tanzania, wazalishaji wa bidhaa za Tanzania walilazimika kwenda nje ya nchi kutafuta ‘barcodes’ ili kuwawezesha  kuuza bidhaa zao katika masoko ya ndani na yale ya kimataifa.

Waziri Mkuu alisema hali hiyo iliifanya Tanzania kuwa wategemezi na kuchangia kuzalisha ajira kwa ajili ya nchi nyingine kwa kununua ‘barcodes’ zao. </p><p>“Tangu kuanzishwa kwa chombo chetu, tumejinasua kutoka katika utegemezi huo,” alisema.

Pia waziri mkuu alisema amefurahishwa na mipango iliyowekwa na GS1 Tanzania ya kuhakikisha kwamba mazao ya kilimo yanapatiwa barcodes na kuwaelimisha wananchi kuhusu alama hizo. Mkutano huo ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji,  Stella Manyanya, Waziri wa Viwanda na Biashara wa Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali na  Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Elisante Ole Gabriel.

Wengine ni Mwenyekiti wa Bodi ya GS1 Tanzania Dkt. Gideon Mazara, Wakuu wa Mikoa chiku Galawa (Songwe), Evarist Ndikilo (Pwani) na Christine Mndeme (Ruvuma); wa Taasisi na Wadau wa GS1 kutoka Tanzania Bara na Visiwani (TBS, BRELA, TANTRADE, ZNCIAAL, COSTECH na Mtendaji Mkuu wa GS1 Tanzania, Fatuma Kange.

Source: https://m.ippmedia.com